Unapatikana katikati ya Miji miwili (2) maarufu ya Cairo nchini Misri na Cape Town nchini Afrika Kusini katika umbali wa kilometa 5,233.5. Arusha hutambulika kama kitovu cha sekta ya utalii kipatikanacho Kaskazini mwa Tanzania. Mkoa wa Arusha umejaaliwa kuwa na muonekano mzuri wa kimazingira na wingi wa viumbe hai ikiwemo wanyama na mimea tofauti na ya kuvutia, hali ya hewa iliyo bora na ya kupendeza, watu wenye haiba ya ukarimu pamoja na vivutio vingine vya utalii vikiwemo hifadhi za Taifa ka vile, Arusha, Tarangire, Manyara na Ngorongoro crater ambayo ni moja ya maajabu ya asili ya dunia na chimbuko la mwanadamu wa kale katika bonde la Olduvai ( Olduvai gorge) na pia Arusha ni lango kuu la kuingilia katika mbuga maarufu ya Serengeti.
Katika suala la ufikikaji Jiji la
Arusha ni kama “kitovu cha Utalii” na ni rahisi kufikika kwa njia ya barabara
na anga pia. Kuna Barabara kuu zenye lami, mambazo huleta watu kutoka mikoa
mbalimbali inayoizunguka na ile ilipatikanayo mbali. Pia unaweza kifika kwa
usafiri wa anga kwa kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro na
Uwanja mdogo wa Ndege wa Arusha. Pamoja na hayo Arusha ni sehemu pekee yenye
hoteli nyingi na nzuri pamoja na nyumba za kulala wageni ambazo zinapatikana
kwa viwango tofauti zinazokidhi mahitaji na bajeti ya wageni.
AINA ZA UTALII ZIFANYIKAZO ARUSHA
Pakiwa kama kitovu cha utalii nchini Tanzania, Jiji la Arusha
kulingana na maliasili zipatikazo pamoja mandhari zake tofauti tofauti za
kuvutika, Arusha ni sehemu mojawapo ambayo aina mbalimbali za utalii hufanyika.
Sifa hii imepelekea Jiji la Arusha kupokea wageni wengi kutoka ndani na nje ya
nchi ili kuja kujionea mambo mbalimbali ya kuvutia yanayopatika katika Jiji
hili.
Aina hzo za utalii ni pamoja na:
Aina hzo za utalii ni pamoja na:
·
Utalii
wa mbuga na kuvinjari nyikani
·
Utalii
wa kupanda milima
·
Utalii
wa uwindaji
·
Utalii
wa kitamaduni
·
Utalii
wa ikolojia (Ecotourism)
·
Utalii
wa malikale
·
Utalii
wa mikutano
·
Utalii
wa matibabu
·
Utalii
wa mashambani
·
Utalii
wa miji
ORODHA YA VIVUTIO
VIPATIKANAVYO ARUSHA
Kuwa na volkano isiyo hai , Milima Meru ni wa pili kwa ukubwa
Tanzania ukiwa na kilele kilicho simama
katika futi 14980 ft ( 4566 m) kutoka usawa wa bahari nyuma ya Milima
Kilimanjaro. Mlima Meru wenye muonekano mzuri na rahisi ukiwa katikati ya Mji
wa Arusha, ni moja kati ya milima ipatakanoyo kaskazini mwa Tanzania katika
moyo wa Hifadhi ya Taifa ya Arusha. Mara ya mwisho kutoa volkano yake ndogo,
inasemekana ni zaidi ya karne iliyopita. Unaweza kupata muonekano mzuri na bora
wa Mlima Kilimanjaro kutoka Mlima Meru, kwani ipo chini ya maili 50 kutoka
Milma momja kwaenda mwingine.
Mlama Meru ni chaguo sahihi kwa wale wanaotaka kuchanganya
upandaji wa Milima huku ukishuhudia baadhi wa wanyama pori wakati ukielekea
kileleni mwa mlima. Wakati Milima Kilmanjaro ukiwa ni vigumu kuona wanyama
pamoja na ndege kwa karibu kutokana na kutawanyika kwao, ila hii ni tofauti
uwapo katika miteremko ya Mlima Meru kwani unaweza kuona vyote kwa pamoja kwa
urahisi huku ukiwa unapanda kuelekea kileleni au kushuka. Unaweza kuona viumbe kama Nyati, Twiga, Nyani,
Tembo pamoja na fisi kwa uchache. Kwa wageni wenye bahati wanaweza hata kuwa na
nafasi ya kuona chui wakiwa kwenye vivuli au wakiwa wanaondoka taratibu na
kupotelea machakani wakiepuka kuonekana na viumbe wengine kama binadamu.
Utalii unaofanyika hapa ni Utalii wa upandaji Milima, utalii
wa ekolojia, pamoja na utalii wa kuvinjari nyikani.
Hifadhi ya nyoka ya Meserani inayopatikana Arusha ni hazina
maalum, kwa wageni na wenyeji kwa madhumuni ya kujiburudisha na kustareheka
yenye mazingira ya utulivu. Hifadhi hii ya nyoka iko 25km Magharibi mwa Arusha
kando kando ya barabara kuu ilelekeayo katika mbuga maarufu duniani za
Serengeti na Ngorongoro.
Ukiwa katika Hifadhi ya nyoka ya Meserani unaweza kufanya shughuli
mbalimbali, ikiwemo pamoja na kufanya ziara ya kuongozwa na kujifunza kuhusu
baadhi ya nyoka hatari zaidi duniani, kama vile Black na Green Mamba, Egyptian
Cobra, Kifutu (Puff Adders) na wengine wengi zaidi. Unaweza kupata nafasi yako
ya kupiga picha na kumshika nyoka halisi anayeishi pamoja na kushuhudia Mamba
wenye urefu zaidi ya mita 3 na kuendelea, huku ukipata picha yako ya kumbukumbu
na kitoto cha mamba.
Pia unaweza kufurahia kwa kujifunza tamaduni mbalimbali za
kabila la Kimasaai kwa kutembelea Makumbusho zao pamoja na kupanda Ngamia huku
ukizunguka na kufanya safari katika kijiji kilichopo karibu na eneo hili la
Meserani.
Pia unaweza kufanya ziara katika kituo cha elimu ambapo
Wamasai wanapata nafasi ya kujifunza jinsi ya kusoma na kuandika pamoja na
kujifunza tamaduni zao mbalimbali.
Utalii unaofanyika hapa ni pamoja na utalii wa kitamaduni,
utalii wa kihistoria juu ya makabila ya kimasai pamoja na nyoka hatari zaidi
duniani wapatikanao katika eneo hili.
Hifadhi ya taifa ya
Arusha yenye ukubwa wa kilometa za amraba 328.4, iko umbali wa kilometer 62
kutoka Arusha mjini. Hifadhi hii ina maeneo matatu muhimu ambayo ni; bonde la
ngurudoto (Ngurudoto crater) maziwa ya momella ambayo kila moja hotoa mandhari
tofauti pamoja na Mlima Meru wenye urefu wa mita 4,566 hali ambayo inaifnya
hifadhi hii kuwa na mazingira ya baridi na ya kuvutia.
Viumbe mbalimbali
hutumia hifadhii hii kama makazi yao muhimu, baadhi ya viumbe hao ni kama mbega
weusi na weupe. Wanyama wengine wanaopatikana kwa wingi katika hifadhi hii ni
pamoja a pundamilia, nyati, tembo na digidigi. Aidha unaweza kuwaona chui
wakiwa kwenye vivuli vya miti pamoja na makundi kadhaa ya bata maji wakitafuta
malisho katika maziwa ya momella. Vilevile hifadhii ni imethibitika inatunza
zaidi ya aina 400 za ndege wa aina mbalimbali.
Aina za utalii
zinazofanyika katika hifadhi hi ni pamoja na Utalii wa mbuga na kuvinjari nyikanii,
Utalii wa majini katika Maziwa ya Momella, utalii wa kupanda Mlima hususani Milima
Meru, Utalii wa ekilojia (ecological tourism) pamoja na Utalii wa kupiga picha.
Hifadhi ya Taifa ya
Ziwa Manyara ni kovutio kingine kinacho lipamba Jiji la Arusha na kuzidi
kukamilisha sifa yake ya kuwa kitovu cha ualii Nchini. Hifadhi ya Ziwa Mnayara
ni maarufu sana nchini kwa samba wapandao miti. Hifadhi hii inapatika ndani ya
Bonde la ufa ambalo kingo zake zinaongeza mandhari nzuri katika Hifadhi hii.
Wageni kutoka ndani na nje ya Nchi huja kutembelea hifadhi hii na kujionea
maajabu ya dunia haswa viumbe wa porini (wanyama, mimea na ndege). Wanyama
wanaopatika katika hifadhi hii ni pamoja na simba, nyati, tembo, chui,
pundamilia na wanyama wengine walao majani na nyama. Hifadhi hii inasifika pia
kwaa wingi wa ndege haswa heroe, na mnandi ambao wanaonekana katika makundi makubwa
na kufanya eneo hili la kitalii kuwa na zaidi ya aina 400 za ndege.
Vilevile hifadhi
hii inatunza chemchem ya maji ya moto ambayo ni moja ya maajabu yapatikanayo
katika hifadhi hii na inayovutia wageni wengi. Kwa mamilioni ya miaka, maji hayo
yamekuwa yakibubujika kutoka ardhini na huonekana yakitoa mvuke kama maji
yanayochemka jikoni.
Aina za utalii
zinazofanyika katika Hifadhi hii yaTaifa ni pamoja na Utalii wa mbuga na
kuvinjari nyikanii, Utalii wa ekilojia (ecological tourism) pamoja na Utalii wa
kupiga picha.
Hifadhi ya Taifa ya
Tarangire ni maarufu kwa makundi makubwa ya tembo wanaoweza kuonekana katika
eneo dogo. Tarangire pia ina mandhari nzuri ya kuvutia yanayotokana na maumbile
ya mibuyu inayosadikwa kuwa na umri zaidi ya miaka eflu nne.
Wanyama
wanaopatikana ndani ya hifadhi hii ni pamoja na pundamilia, nyumbu, swala, simba
nyati, kongoni, chui, duma na wengineo wengi. Pia Hifadhi hii ni maarufu kwa
ndege ambayo zaidi ya aina 550 za ndege zimerikodiwa katika eneo hili. Mbali na
yote hifadhi hii ni maarufu kwa upatikanaji wa chatu wakubwa walio na uwezo wa
kukwea miti. Ni kutokana na umaarufu wa hifadhi hii idadi ya wageni
wanaotembelea hifadhi hii imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.
Mto Tarangire ni
mto ambao hutiririsha maji yake kipindi chote cha mwaka, kitu ambacho
kimeufanya mto huu kuwa kimblio la wanyama wengi wapatikanao katika hifadhi hii
hususani kipindi cha ukame wakati mvua hazinyeshi na kupelekea vijito vingine
kukauka. Hii pia hupelekea zoezi la kuona wanyama kuwa rahisi kutokana na
kuzingira mto huu kwa ajili ya kunywa maji na mawindo pia hususani kwa wanyama
walao nyama kama simba.
Aina za utalii
zinazofanyika katika Hifadhi hii ya Taifa ni pamoja na Utalii wa mbuga na
kuvinjari nyikanii, Utalii wa ekilojia (ecological tourism) pamoja na Utalii wa
kupiga picha.
Ni moja ya
makumbusho zinazopatikana katikati ya jiji la Arusha inayopatikana barabara ya
Boma karibu na ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa AICC, ofisi za Manispaa
pamoja na ofisi za Mkoa Arusha. Makumbusho ipo kwenye Boma iliyojengwa na
Wajerumani katika miaka 1900 iliyokuwa ikitumika kama jengo la Utawala na
mawasiliano wakatiki wa ukoloni wa Kijerumani wakati huo nchi ikijulikana kama
Tanganyika.
Makumbusho ilifunguliwa rasmi mnamo mwaka 1987 na kuonesha
historia ya binadamu wa kale, ikiwepo pamoja na tafiti zilizofanyika katika
bonde maarufu la Olduvai (Olduvai Gorge) na alamaza za miguu wa binadamu wa kale
za Laetoli (Laetoli footprints). Pia inafanya Maonyesho juu ya entomolojia
ambayo huwasilisha baadhi ya wadudu, ndege na wanyama pamoja na umuhimu wao
kiuchumi ambacho pia ni kivutio kikubwa kwa wageni wanaotembelea makumbusho
hii.
Makumbusho ya Azimio
la Arusha iko katika
eneo la Kaloleni katika Jiji la Arusha. Ni ya kwanza kabisa kati ya makumbusho
zilianzishwa katika mkoa wa Arusha na mzunguko wa kiutalii wa kaskazini mwa
Tanzania. Makumbusho hii ipo katika jengo la kihistoria ambalo mpaka mwaka 1967
lilitumika kama jengo la ustawi wa jamii na ukumbi kwa ajili ya watu wa eneo la
Kaloleni. Makumbusho hii ilipata kufunguliwa kwa umma mnamo mwaka 1977 na hasa
ilionesha historia ya kisiasa ya Taifa letu. Baada ya kutembelea makumbusho hii
utaona picha ya uundaji wa sera ya kujitegemea, mapambano kwa ajili ya uhuru,
historia ya Ukoloni, na maendeleo ya kisiasa ya Tanzania.
Ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) ulianzishwa tarehe
25 Agosti 1978. Uwepo wa ukumbi huu unafanya Jiji la Arusha kuongeza idadi
zaidi za aina za Utalii zinazofanyika katika Jiji hili ukiwemo Utalii wa
Mikutano. Ukumbi huu ni mkubwa na umekuwa ukifanya mikutano mbalimbali ya
kiserikali na taasisi binafsi kutoka ndani na nje ya nchi. AICC unabaki kama
ukumbi na alama muhimu ya utalii katika Jiji la Arusha.
Oldoinyo Lengai yenye maana ya “Mlima wa Mungu” katika lugha ya Kimasai wenye urefu wa Mita 2962
juu ya usawa wa bahari, na ndio Mlima pekee wenye volkano hai unaopatikana
Tanzania. Kumbukumbu ya milipuko mkubwa zaidi wa Milima Oldonyo Lengai ulitokea
mnamo mwaka 1883, ambao ulirusha majivu yake kwa umbali wa kilomita 100 Kaskazini
Magharibi kwa upande wa Loliondo katika mipaka ya Kenya. Kabila maarufu la
Kimasai hutumia Mlima huu kwa kufanya ibada zao za kimila wakiupa sifa za Uungu
kwa ajili ya kutatua matatizo yao ya kijamii yanayo wakumba kila siku kama
ukame na magonjwa.
Utalii uanofanyaika hapa ni utalii wa kupanda milima.
Ni ziwa lenye maji
ya chumvi linalopatikana kati ya genge la bonde la ufa na na Milima ya Kidero.
Maeneo yazungukayo ziwa Eyasi ni makazi ya kabila maarufu la Wahadzabe ambao ni
moja ya makabila machae ya wawindaji yaliyobaki katika bara la Afrika.
Wahadzabe wamekuwa wakiishi katika misitu ya acacia na vichaka vinavozunguka
maeneo ya ziwa Eyasi kwa atakribani zaidi ya miaka 10,000 iliyopita.
Utalii unaofnyika
katika eneo hili ni utalii wa kitamaduni,
Maeneo yanayozunguka Ziwa Natron yana baadhi ya mazingira ya
kushangaza zaidi barani Afrika. Mazingira hayo ni pamaoja na mchanganyiko wa
maeneo mpana ya wazi na tambarare, miinuko, Mlima mkubwa wa volkano pamoja na
ziwa lenyewe lenye asili ya madini soda yenye rangi mbalimbali, ni dhahiri
kwamba eneo hili ni la kuvutia na kupendeza.
Umuhimu wa ziwa
hili katika ukanda wa Afrika Mashariki unatokana n ukweli kwamba ndio sehemu
pekee katika ukanda huu ambapo panatoa fursa ya ndenge aina ya flamingo
kuzaliana kwa wingi.
ENGARUKA
Engaruka inapatikana kilometa 63 kaskazini mwa Mto wa mbu katika barabara ya Oldnyo lengai na ziwa Natron chini kidogo ya genge (escapment) la bonde la ufa. Ni sehemu muhimu ya kihistoria kama inavosemekana miaka 500 iliyopita jamii ya wakulima ya watu elfu kadhaa waliamua kuendeleza kilimo cha umwagiliaji katiaka eneo hili, ila, kwa sababu zisizo julikana wakulima hao waliondoka Engaruka miaka 1700 iliyopita na kuacha magofu ambayo mpaka sasa yanaongelea ni jinsi gani sehemu hii iliendelea kwa kufanya kilimo cha kisasa kwa ajili ya uchumi wao na chakula.
Utalii unaofanyika
katika eneo la Engaruka ni utalii wa Kihistoria, na kitamaduni juu ya jamii ya
wakulima iliyopata kuishi katika eneo hili miaka 1700 iliyopita.
Ziwa Duluti ni ziwa
dogo lenye asili ya kivolkano (crater lake) ambalo ni kivutio kingine
kinachopatika katika Jiji la Arusha nje kidogo ya Jiji katika mji mdogo wa Tengeru
likiwa limezungukwa na msitu mzuri wa asili penye mazingira tulivu penginre
kuliko sehemu yeyote ile uliopata kuwa. Ziwa lipo katikati ya msitu mnene wenye
mimea mbalimbali ya mwituni pamoja na viumbe hai vingine vikiwemo ndege kama
vile Kingfisher, Buzzard, Mnandi, Njiwa, na Barbet na wanyama mbalimbali. Eneo
hili linatoa shughuli mbalimbali za kitalii kama vile michezo ya uvuvi, kupanda
mtumbwi, matembezi ya mwituni kwa ajili ya kuangalia ndege wazuri wapatikao
katika msitu wa ziwa Duluti.
Utalii unaofanyika
Ziwa Duluti ni pamoja na utalii wa kwenye maji, utalii wa ekolojia (eco
tourism), utalii wa matembezi nyikani.
NGORONGORO CRATER
Ukitokea barabara
ya Manyara kuelekea Ngorongoro utapanda mlima mkali uliopo kwenye kuta za bonde
la ufa na usifanye kosa la kuacha kutazama mandhari nzuri ya bonde la ufa
ufikapo juu. Baada ya hapo utapita katika plateu ya mbulu penye barabara za
mianda ambayo ni maarufu kwa kilimo kinachofanywa na watu wa mbulu maarufu kama
wairaq. Mbele kabisa kuna msitu mnene uliopo kwenye muinuko mkali ambao ni
upande mmoja wa Ngorongoro crater, ambapo pengine hujulikana kama kimbilio
maarufu zaidi la wanyama pori duniani. Ukiwa juu ya mzunguko wa creter kwa
urefu upatao mita 2400 (futi 8000) na uangaliapo chini utaona sehemu kubwa enye
nyasi, misitu pamoja ziwa.
Ngorongoro crater
ni moja ya maajabu ya asili ya dunia sehemu inayojulikana zaidi kwa wingi wake
wa viumbe hai mbalimbali vya porini na ndio sababu pekee ambayo sehemu hii
imekuwa ikiiwavutia wageni wengi kutoka ndani na nje ya nchi. Ingawa Ngorongoro
crater in sehemu ndogo ya Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro ambayo inatoa fursa
ya kushuhudia aina tofauti za vivutio vya kitalii kwa wageni wake.
Upekee wa
Ngorongoro hutokana na ukweli kwamba, inachanganya historia ya wanadamu na
muingiliano wa mazingira yake hususani wanyama pori katika eneo moja bila
kuathiriana, kitu ambacho kimekuwa ni kigumu kwa sehemu nyingi Afrika na dunia
pia.
Aina za utalii
zinazofanyika hapa ni pamoja na Utalii wa mbuga na kuvinjari nyikani, Utalii wa
ekilojia (ecological tourism), utalii wa kitamaduni na historia, pamoja na
Utalii wa kupiga picha.
Katika kipindi cha
miaka thelathini iliyopita, imekuwa wazi kuwa pengine Bara la Afika ndilo chimbuko
la mwanadamu. Kutoka katika Bara hili ndipo walipoanza kuenea na kutawanyika na
kujaza maeneo mengine duniani. Hii ni kutokana na tafiti zilifanywa na
kupatikana kwa mabaki ya binadamu wa kale katika eneo la Bonde la Olduvai
(Olduvai Gorge) katika Mkoa wa Arusha.
Bonde la Oldupai
(mwanzo likitamkwa kama Olduvai) ni eneo maarufu zaidi la Kiakiologijia
lipatikanalo Afrika ya Mashariki ambalo limekuwa kivutio muhimu kwa watilii
wengi wajao ukandaa huu wa Afrika ya Mashariki hususani pindi wajapo Ngorongoro
au wakiwa wanaelekea katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Pia ni sehemu muhimu
ya kujifunza juu ya historia ya mwanadamu wa kale kwa watalii wa ndani watokao
sehemu mballimbali ya nchi.
Tupo tayari kuwajulisha juu ya uzuri wa nchi yetu ya Tanzania, na kuvitangaza vivutio vyote vya utalii vinavopatikana hapa nchini. Kaa tayari kupokea na kuvijua vivutio vingine vipatikanavyo katika Mkoa mwingine wa Tanzania hivi karibuni.
Kama ilivYo ada, kaulimbiu yetu siku zote ni "UTALII KWA WOTE"
Tupo tayari kuwajulisha juu ya uzuri wa nchi yetu ya Tanzania, na kuvitangaza vivutio vyote vya utalii vinavopatikana hapa nchini. Kaa tayari kupokea na kuvijua vivutio vingine vipatikanavyo katika Mkoa mwingine wa Tanzania hivi karibuni.
Kama ilivYo ada, kaulimbiu yetu siku zote ni "UTALII KWA WOTE"